Nina jingi jakamoyo, linonipiga katiti
Kulitowa kwenye moyo, yabidi nijizatiti
Maana kwa wengi siyo, wana nyingi ati ati
Hakuna penzi la dhati, sihadaiwe na mtu!
Pendo usiliasisi, ukaliona ni fiti
Mwenye nalo yuna nuksi, huweza kukusaliti
Ni ndugu zake Yudasi, na wanazo ithibati
Hakuna penzi la dhati, sihadaiwe na mtu!
Moyo una nyingi siri, kingi kizungumkuti
Uahidiwe sayari, na nyama kwa sharubati
Kwenye ndoto utajiri, siwe mwepesi kubeti
Hakuna penzi la dhati, sihadaiwe na mtu!
Wengi wana nia zao, na njama za kukuseti
Ukishatekwa na wao, ushindwe kujithibiti
Mwisho ukapinda tao, na kujikuta maiti
Hakuna penzi la dhati, sihadaiwe na mtu!
“Kimwana umerembeka, wawaka ja kiberiti
Nakupenda ni hakika, nina nawe mikakati”
Hayo mafamba epuka, utapigwa mabaluti
Hakuna penzi la dhati, sihadaiwe na mtu!
Yapo mengine mabusu, kama ya Iskaryoti
Alivyofanyiwa Yesu, kauzwa senti thalati
Lahitaji udurusu, penzi la kupigwa goti
Hakuna penzi la dhati, sihadaiwe na mtu!
Kwa hili fungu la saba, ndipo nakomesha beti
Penzi ni kama msiba, ukishatendwa na switi
Moyo utakosa tiba, onyo la bwana Sereti
Hakuna penzi la dhati, sihadaiwe na mtu!
© Limehaririwa Jumanne 25.02.2025