Jumapili, 11 Agosti 2013

NYOTA YANGU

Nyota yangu ya thamani, nahitaji kukuona
Umenikaa moyoni, bila wewe sitapona
Wapotelea gizani, ninapolala kichuna!
Nyota yangu ya usiku, nakutamani mchana!

Nimeshindwa kutulia, na imenikumba suna
Usiku kukungojea, nguvu za kukesha sina!
Ghafula ninasinzia, kwa usingizi wa kina
Nyota yangu ya usiku, nakutamani mchana!

Mchana nina nafasi, mie nawe kuonana!
Tujilaze kwenye nyasi, ya moyoni kuyanena
Twondowane wasiwasi, mawazo kutulizana!
Nyota yangu ya usiku, nakutamani mchana!

Mwangaza wako wa shani, wanijaza uchu sana!
Ndio ninaotamani, kwenye anga la mchana
Nakuomba niauni, nyota yangu ya maana!
Nyota yangu ya usiku, nakutamani mchana!

Giza linapoingia, wenzi wananitukana
Shere wananifanyia, ndoto yangu kuibana
Bali nitavumilia, madhali tunapendana!
Nyota yangu ya usiku, nakutamani mchana!

Kigae cha almasi, uso uliojipuna
Nakomea hapa basi, nimejua hutanuna!
Ushindane na shamsi, usiku ung'ae tena!
Nyota yangu ya usiku, nakutamani mchana!

BIN-ADAM

Nina kauli-kinzani, peupe naianika!
Ituhusuyo insani, na sifa tunojivika
Majigambo midomoni, mwenzi-kwa-mwenzi mipaka!
Kama u safi, taulo, inachafuka kwa nini?

Tajiri na masikini, wapi wote walitoka?
Kujigamba na mapeni, jumba, gari, madaraka!
Mkata mwenye huzuni, isitoshe wamcheka!
Kama u safi, taulo, inachafuka kwa nini?

Nayaingilia ndani, naomba kueleweka!
Unapoenda bafuni, kukoga ukasafika
Wapangusa maungoni, na marashi kujipaka
Kama u safi, taulo, inachafuka kwa nini?

Urembo wako mwilini, aliokupa Rabuka
Unakufanya huoni, wengine ni takataka!
Usifanye uhaini, mawaidha kutapika
Kama u safi, taulo, inachafuka kwa nini?

Ningeishi mawinguni, ningekuwa malaika!
Kuliko ulimwenguni, huku kulikochafuka!
Mtu ni utu jamani, bure unachacharika!
Kama u safi, taulo, inachafuka kwa nini?

Towa nta sikioni, binadamu msifika
Alotuumba Manani, duniani katuweka
Pua zyangalie chini, na ndipo tulipotoka
Kama u safi, taulo, inachafuka kwa nini?

 Nenda zangu Msituni, nikiwa nimeudhika
Bali furaha moyoni, kwa ujumbe kunitoka!
Sote tujivishe soni, ja nguo zimeraruka!
Kama u safi, taulo, inachafuka kwa nini?

SILI NYAMA YA NGURUWE!

Sili nyama ya nguruwe, leo nimeitambua!
Nimeikana mwenyewe, bila mtu kunambia!
Inanitia kiwewe, pia inanichafua!
Ni 'nyama mwenye udhia, sili nyama ya nguruwe!

Silazii nipikiwe, mboga zijapokosea
Hamu isinizuzuwe, zama nikikumbukia
Muwele sitaki niwe, nilokula yatoshea!
Ni 'nyama mwenye udhia, sili nyama ya nguruwe!

Nilisoma nimwelewe, kwa nini twamchukia!
Mola hataki aliwe, Qur'ani na Biblia
Mbali akatupiliwe, alipo kupakimbia!
Ni 'nyama mwenye udhia, sili nyama ya nguruwe!

Wacha mbwa wapikiwe, wao watafurahia!
Sitaki nipambaniwe, Jehannam n'kaingia
Na kwangu asifugiwe, sina chembe ya hisia
Ni 'nyama mwenye udhia, sili nyama ya nguruwe!

Harufu yake nguruwe, pote anapopitia
Ataka mumtambuwe, msipomuangalia
Ni benibeni mwendowe, tapishi kwake halua!
Ni nyama mwenye udhia, sili nyama ya nguruwe!

Ni vyema nikashifiwe, na wenzangu familia
Wala cheo nisipewe, kundi kulisimamia!
Bali kufuga nguruwe, nimekana niachia!
Ni 'nyama mwenye udhia, sili nyama ya nguruwe!

Kwa mafuta asifiwe, na juhudi kitabia
Kila kitu akijuwe, anuse na kujilia
Atamani mbele awe, kwanza mapya kupokea!
Ni 'nyama mwenye udhia, sili nyama ya nguruwe!

Watalii wachinjiwe, uchu kuwaondolea!
Filamu wachukuliwe, wa ng'ambo kupelekea!
Ama mbwa wapikiwe, na punda kufurahia!
Ni 'nyama mwenye udhia, sili nyama ya nguruwe!

Kitambo niing'wafuwe, sikuwa nimeijua!
Sasa leo iepuwe, ni haramu nisikia!
Mara ngapi muambiwe, kwamba ni mbaya! Yaua!
Ni 'nyama mwenye udhia, sili nyama ya nguruwe!

Yanipa maruweruwe, ijazwapo sufuria!
Nashindwa vipi iliwe, na mbwa waingojea!
Ninakoma nipumuwe, ujumbe huu pokea:
Ni 'nyama mwenye udhia, sili nyama ya nguruwe!

JERAHA LA MOYO

Moyoni nimeumiya, nimepagazwa kupenda
Juhudi nilizotiya, tiarangu kuiunda
Hewani kuitezeya, na upepo ikaenda!
Kukosa ulichopenda, rahisi kukichukiya!

Angani ilipo'ngiya, eneole ikatanda
Uzi nikaachiliya, 'kadhani itajipinda
Nyuma kuifatiliya, tiara 'kazidi kwenda!
Kukosa ulichopenda, rahisi kukichukiya!

Wapi imepoteleya, tiara niliyopenda?
Vipi nitaifikiya, na kupaa kwanishinda?
Ni hofu kuvumiliya, na jinsi nilivyokonda!
Kukosa ulichopenda, rahisi kukichukiya!

Mlo nazo 'sinambiya, nimeapa kutopenda!
Tiara zina kayaya, kupozi nazo kwa inda!
H'wenda ikawa kinaya, dhidi ya pepo 'zilinda!
Kukosa ulichopenda, rahisi kukichukiya!


Ahsante sana hewala, kwa auni za busara!
Nilikuwa nimelala, nikiwaza kwa hasira
Bali nasema Inshalla! Nitaipata tijara!
Nilomsifu "Tiara", kwangu ameshakugura!


 Pishi nashindwa kulila, pendo halina sitara
Chumba tulopamba sala, nakiona ja ahera
Mola ukiwa ni hila, nipe mwengine kisura!
Nilomsifu "Tiara", kwangu ameshakugura!


Nimelingana kwa Mola, atujeze maghufira
Apate alo aula, nami nimpate bora
Mambo yasiwe ghafula, huvuta heri subira!
Nilomsifu "Tiara", kwangu ameshakugura!


DIWANI YA MRATIBU, 2013. 

HII KENYA, KENYA GANI?

Nina hasira moyoni, nimeshindwa vumiliya!
Namsaili Manani, satuwa kusubiriya
Visa tuliona Pwani, kamwe visijerudiya!
Mbwa-mtu tangu lini, "mapenzi" kuyadoweya?

Kaja huyo Baniani, mapeni kuwapatiya
Na kamera mkononi, mbwa kamfunguliya!
Mabinti zetu jamani, mbona soni mwajitiya?
Mbwa-mtu tangu lini, "mahaba" kuyatezeya?

'Wapenzi' niambiyani, nisije potoka njiya
Mbona tumejilaani, kwa nyendo zilopoteya?
Hii sasa Kenya gani, mahoka twajitupiya?
Mbwa-mtu tangu lini, "ngono" wakafurahiya?

Nema mbiu napigani, naomba mnisikiya!
Mili yetu ya thamani, maradhi jiepushiya!
Mabinti nanyi mabini, rekebisheni tabiya!
Mbwa-mtu tangu lini, kitanda kujilaliya?


Nimefurahi wendani, kwa hili kulitangiya
Sote tukaunganeni, tuipige vita haya!
'Tendo la uhayawani, unajisi latutiya:
Mbwa-mtu tangu lini, nikaha kushirikiya?


Glen umebusuri, ni bora huyo wa Nyeri
Mie naona ni heri, ameikata dhakari!
Kilema uwe vizuri, mzima uchomwe nari!
Mbwa-mtu tangu lini, sahani moja kuliya?


 Namunukuu Karima, kwa neno la Bibliya:
"Ni bora uwe kilema, mbinguni ukaingiya
Kuliko kuwa mzima, Jehannum kupoteya!"
Mbwa-mtu tangu lini, kudongozaniya njiya?

MKAMIA MAJI

Ni kipi kinokuliza, mayowe twayasikia?
Walia kufululiza, 'kitweta kila hatua!
Huwajali watuliza, sikio 'mewazibia!
Uwache kukililia, usichoweza kupata!

Mtu akikutuliza, uwache kumfokea
Bila ya kumfukuza, ni vema kumsikia!
Ujapokosa nyamaza, wacha tishiatishia!
Uwache kukililia, usichoweza kupata!

Ndugu epuka matata, nakupa huu wosia
Kwa udi kutotafuta, makuu kujitakia
Unajigamba u jeta, utu umeshauvua!
Uwache kukililia, usichoweza kupata!

Waparamia mafuta, ki ki ki washikilia
Jaala hutoifuta, aloandika Jalia!
Mpiga ngumi ukuta, makono yataumia!
Uwache kukililia, usichoweza kupata!


(DIWANI YA "MRATIBU", 2013).