Jumatano, 21 Agosti 2013

SIKU YANGU

Ningekuwa na mabawa, kama ndege ningeruka
Nifike kwenye maziwa, penye misitu na nyika
Kumshukuru Moliwa, aloniongeza mwaka
Mwakani naikumbuka, siku niliyozaliwa!

Shaabani ilikuwa, themanya-sidusi mwaka
Ishirini-tatu chwewa, mapema kupambazuka
Fatiha ikajibiwa, myezi kenda kutimika
Mwakani naikumbuka, siku niliyozaliwa!

Nisaidieni njiwa, makero kutambilika
Swala njema kuombewa, kwa khatwiri ya shufaka
Mema piya kutakiwa, nyoyonimwe wahibaka
Mwakani naikumbuka, siku niliyozaliwa!

Vinono nikichinjiwa, siwezi nikaridhika
Dengeluwa kujaziwa, na keki za kubanika
Nishirikishie duwa, kwa Mola na malaika!
Mwakani naikumbuka siku niliyozaliwa!

SHEREHE ZA KUADHIMISHA MWAKA WANGU WA 25.
KWA WAPENZI WANGU WOTE WENYE NIA NJEMA NA DHAMIRI.

HONGERA KISURA!

Nema naja jukwaani, kuikatisha subira!
Niseme yalo moyoni, tuloshushiwa ghufira
Nipokeze shuqrani, shule'etu kutia fora!
Bibi Tabitha hongera, uongoze shule yetu!

Wahitaji shuqrani, Tabitha wetu kisura
Matokeo ya mwakani, tukapata kumi bora
Siwavalii miwani, walimu wetu hongera!
Bibi Tabitha hongera, uongoze shule yetu!

Ulotenda mhisani, shuleni siyo hasara
Mikataba kusaini, vitabu tukavidara
Kapita madarasani, ukapeana busara
Bibi Tabitha hongera, uongoze shule yetu!

Makelele vidatoni, walokuwa kuzurura
Walopoteza imani, wote kawapa tijara
Akaziweka kanuni, zikasimama imara!
Bibi Tabitha hongera, uongoze shule yetu!

 Makelele vidatoni, walokuwa kuzurura
Walopoteza imani, wote kawapa tijara
Akaziweka kanuni, zikasimama imara
Bibi Tabitha hongera, uongoze shule yetu!

Toka juu hadi chini, aliunganisha dira
Walimu wa afisini, wakatuvunjia nira
Tukaingia vitani, tukaacha masihara
Bibi Tabitha hongera, uongoze shule yetu!

Wazazi waliamini, wakavaa matambara
Mwana aende shuleni, kujiundia ijara
Leo tupo shereheni, wazazi wetu hongera!
Bibi Tabitha hongera, uongoze shule yetu!

 Vitabu maktabani, na kujengwa maabara
Ni mwanzo wa tumaini, kujaliwa madhukura
Tuingie masomoni, tuitimize ishara
Bibi Tabitha hongera, uongoze shule yetu!

Asante wetu wageni, mumetujaza fikara
Kupita ni letu deni, nawaombea subira
Sikusahau Diwani, Bibao George Morara
Bibi Tabitha hongera, uongoze shule yetu!

Wanafunzi jikazeni, msije mkatukera
Muingie vyuoni, tufukuze ufukara!
Kerongorori jamani, siku zote tukang'ara!
Bibi Tabitha hongera, uongoze shule yetu!

 Malenga wa Msituni, niwapokeze taswira
Mwaka huu hamsini, watafata taashira
Mola utupe hisani, tufyatuke ja kombora!
Bibi Tabitha hongera, uongoze shule yetu!

KWA MWALIMU MKUU,
BI. TABITHA MOGONCHI,
SHULE YA MSETO, KUTWA NA MALAZI - UPILI, KERONGORORI.
(Shairi hili, nililitunga na kulighani nikiwa mwanafunzi kidato cha nne, katika sherehe SIKUKUU YA TUZO, Mei 15, 2009).

KAZI YANGU (MAHASIDI)

Kazi yangu ya mikono, ndugu nishapowambia
Ni mshipi wa kiuno, nitakapojifungia
Mbona yenu minong'ono, pote mnapotembea?
Mbona mnajisumbua, nifanyapo kazi yangu?

Finyango nazofinyanga, Mola amenijalia
Mbona msipojitenga, matusi mwanitupia?
Kwa nini mnanipinga, mwanisengenyea pia?
Mbona mnajisumbua nifanyapo kazi yangu?

Wema tenda zako nenda, wahenga walitwambia
Yenu mnayoyatenda, ni nani mtagaia?
Kazi yangu nayopenda, mbali mwaitupilia!
Mbona mnajisumbua, nifanyapo kazi yangu?

 Kama mngekuwa wema, auni kunichangia
Mnipe busara njema, nami ningewaungia
Sasa mwaipanga njama, mwataka kuniulia!
Mbona mnajisumbua, nifanyapo kazi yangu?

Mmenisumbua sana, mori imenipandia
Sipendi kufarakana, na watu wasio njia
Mwajifanya mnaona, hamnazo kujitia
Mbona mnajisumbua, nifanyapo kazi yangu?

Kaditama wa tamati, utunzi kumalizia
Hela nenda jizatiti, kazi zenu jifanyia
Naitwa Nema Sereti, ujumbe nawatilia
Mbona mnajisumbua, nifanyapo kazi yangu?

DIWANI YA "UREMBO WA NEMA, 2003".

MPENZI, NAKUPA MOYO

Wapo wanaotafuta, wa kumpenda hawana!
Wewe ndiwe nilipata, maishani kupendana
Ashiya wa bukhrata, hatima ya kukutana
Ingawaje mali sina, mpenzi, nakupa moyo.

Usiyependa maringo, majigambo wewe huna
Umbole la mviringo, alilokupa Rabana
Una ya upanga shingo, nywele zilizojichana
Mrembo wangu Regina, mpenzi, nakupa moyo!

Sura yako afya kwako, hata ujipake hina
Roho ya mtu iliko, ndiko kwenyeye hazina!
Nema nimetuwa kwako, azizi Wango Regina
Nitakachokupa Nana, Mpenzi, nakupa moyo!

Kila mara nakuwaza, usiku hata mchana
Ndiwe ninayetukuza, bila wewe raha sina
Usije kunipuuza, mpenzi sinitukana!
Kusudi kutulizana, Mpenzi, Nakupa moyo!

Kila mara nakuwaza usiku hata mchana
Ndiwe ninayetukuza, bila wewe raha sina
Usije kunipuuza, mpenzi sinitukana!
Kusudi kutulizana, Mpenzi, Nakupa moyo!

Wango kito cha thamani, ni wewe mwengine sina
Nipe raha maishani, tuishi tukipendana
U malaika wa shani, huna wa kumfanana!
Umenipendeza sana, Mpenzi, Nakupa moyo!

Mwisho nanga naitia, kukuimbia Regina
Leo nakufichulia, Nema nakupenda sana!
Tuhifadhi yetu ndoa, Mola akatupe wana!
Mimi nawe twatoshana, Mpenzi, Nakupa moyo!


KWA MKE WANGU MPENDWA,
REGINA WANGO NEMA,
"KUMBUKUMBU ZA NDOA YETU - MIAKA MIWILI"
Julai 17, 2012.