Jumapili, 18 Mei 2025

MCHAFUKOGE

Nguruwe nilimcheka, alipodara sakafu

Panya 'kamega mkeka, kutanga uharibifu

Mbona twavuka mipaka, vitendo vya uzinifu

Ukikogea machafu, hutakati; utanuka!

 

Ghulamu nyele kusuka, vipini, hina, mikufu

Mihadarati 'bazoka', twatafuna tafutafu!

Twajenga kwenye mizuka, twapitwa na uraufu!

Ukikogea machafu, hutakati; utanuka!

 

Mabinti mmtekeka, 'vinyo kali na midafu

Mavazi mnojivika, yadhihiri maumbifu

Vichusi mnaatika, hamchi Mtakatifu!

Ukikogea machafu, hutakati; utanuka!

 

Usiri huu pulika, epukeni udhurifu

Wenye haiba twataka, hodari sio dhaifu!

Watetezi kadhalika, waungao unadhifu

Ukikogea machafu, hutakati; utanuka!

 



Limehaririwa Alhamisi 10, Mei 2015.

Jumapili, 11 Mei 2025

PONGEZI MAMANGU!

Kutunga ni yangu haja, nisifu mama mzazi

Leo mama nakutaja, tena nikupe pongezi

Ukanizaa miuja, tumboni kenda miezi

N’ambie tunu azizi, nikampe mama yangu!


‘Linifanyia natija, nivaazo na malazi

‘Kanipikia mrija, kunywa uji kwa viazi

Tena ukanipembeja, niupate usingizi

N’ambie tunu azizi, nikampe mama yangu!


Nilipolia ukaja, kunitolea tatizi

‘Kanipapasa mapaja, kunilaza kwa ujuzi

Ukaniimbia luja, nilipokosa tulizi

N’ambie tunu azizi, nikampe mama yangu!


‘Kanijengea daraja, nisome nikamaizi

Leo Napata faraja, najua zile na hizi

Mama napanga lahaja, zizi hizi kumbukizi

N’ambie tunu azizi, nikampe mama yangu!


Sitasema ngojangoja, kukufidia mzazi

Mimi nawe kwa pamoja, ndimi wako mtetezi

Nijapokupa korija, ninaona sikujazi

N’ambie tunu azizi, nikampe mama yangu!


Nipasulie viroja, kama wataka ghawazi

Nitimie niwe mja, mama, nikupe Feruzi?

‘Takujazia mkaja, chapati na maandazi

N’ambie tunu azizi, nikampe mama yangu!



**************************************

(Utunzi wa: Sereti M. Nema, Malenga wa Msituni, Diwani ya Uzindushi, 2009).

Kumbukumbu kwa Sikukuu ya Akina Mama, japo mama aliaga dunia Januari 14, 2024, daima nitadumu kumshukuru kwa kunizaa, kunilea na kunifundisha.

Jumapili 11 Mei, 2025.


#HAPPYMOTHERSDAY

#MyMotherMyHero

#Kisiki

Ijumaa, 9 Mei 2025

MAPENZI HAKUNA!

Nina jingi jakamoyo, linonipiga katiti

Kulitowa kwenye moyo, yabidi nijizatiti

Maana kwa wengi siyo, wana nyingi ati ati

Hakuna penzi la dhati, sihadaiwe na mtu!


Pendo usiliasisi, ukaliona ni fiti

Mwenye nalo yuna nuksi, huweza kukusaliti

Ni ndugu zake Yudasi, na wanazo ithibati

Hakuna penzi la dhati, sihadaiwe na mtu!


Moyo una nyingi siri, kingi kizungumkuti

Uahidiwe sayari, na nyama kwa sharubati

Kwenye ndoto utajiri, siwe mwepesi kubeti

Hakuna penzi la dhati, sihadaiwe na mtu!


Wengi wana nia zao, na njama za kukuseti

Ukishatekwa na wao, ushindwe kujithibiti

Mwisho ukapinda tao, na kujikuta maiti

Hakuna penzi la dhati, sihadaiwe na mtu!


“Kimwana umerembeka, wawaka ja kiberiti

Nakupenda ni hakika, nina nawe mikakati”

Hayo mafamba epuka, utapigwa mabaluti

Hakuna penzi la dhati, sihadaiwe na mtu!


Yapo mengine mabusu, kama ya Iskaryoti

Alivyofanyiwa Yesu, kauzwa senti thalati

Lahitaji udurusu, penzi la kupigwa goti

Hakuna penzi la dhati, sihadaiwe na mtu!


Kwa hili fungu la saba, ndipo nakomesha beti

Penzi ni kama msiba, ukishatendwa na switi

Moyo utakosa tiba, onyo la bwana Sereti

Hakuna penzi la dhati, sihadaiwe na mtu!


© Limehaririwa Jumanne 25.02.2025