Kutunga ni yangu haja, nisifu mama mzazi
Leo mama nakutaja, tena nikupe pongezi
Ukanizaa miuja, tumboni kenda miezi
N’ambie tunu azizi, nikampe mama yangu!
‘Linifanyia natija, nivaazo na malazi
‘Kanipikia mrija, kunywa uji kwa viazi
Tena ukanipembeja, niupate usingizi
N’ambie tunu azizi, nikampe mama yangu!
Nilipolia ukaja, kunitolea tatizi
‘Kanipapasa mapaja, kunilaza kwa ujuzi
Ukaniimbia luja, nilipokosa tulizi
N’ambie tunu azizi, nikampe mama yangu!
‘Kanijengea daraja, nisome nikamaizi
Leo Napata faraja, najua zile na hizi
Mama napanga lahaja, zizi hizi kumbukizi
N’ambie tunu azizi, nikampe mama yangu!
Sitasema ngojangoja, kukufidia mzazi
Mimi nawe kwa pamoja, ndimi wako mtetezi
Nijapokupa korija, ninaona sikujazi
N’ambie tunu azizi, nikampe mama yangu!
Nipasulie viroja, kama wataka ghawazi
Nitimie niwe mja, mama, nikupe Feruzi?
‘Takujazia mkaja, chapati na maandazi
N’ambie tunu azizi, nikampe mama yangu!
**************************************
(Utunzi wa: Sereti M. Nema, Malenga wa Msituni, Diwani ya Uzindushi, 2009).
Kumbukumbu kwa Sikukuu ya Akina Mama, japo mama aliaga dunia Januari 14, 2024, daima nitadumu kumshukuru kwa kunizaa, kunilea na kunifundisha.
Jumapili 11 Mei, 2025.
#HAPPYMOTHERSDAY
#MyMotherMyHero
#Kisiki
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni