Huu ndio mtandao wa kipekee utakaowaauni wapenzi na wakereketwa wa lugha ya Kiswahili. Nimeubuni ili kukuza kipawa, usanii na utamaduni. Utaasika, udadisi na licha ya kuelimika, utaburudika. Usikose kuniachia ujumbe wako, ili nami nijielewe. Asante na karibu.
Jumatano, 14 Agosti 2013
GUGUMAJI (IBILISI MREMBO)
Ziwani linabishana, na samaki ufukweni!
Kwa kasi kuzaliana, bali halina thamani!
Sura huvutia sana, ndani maficho ya jini!
Nimepata nilidhani, kumbe nimepatikana!
Limenitenda kichuna, zogo na purukushani
Usiku hata mchana, sina furaha moyoni
Kufyeka na kuvutana, tabia za kishetani!
Nimepata nilidhani, kumbe nimepatikana!
Juu maji 'kiliona, ni uwanja wa kijani
Chini maji yajazana, kukuhadaa machoni!
Vijinyama vimechina, kukosa okisijeni!
Nimepata nilidhani, kumbe nimepatikana!
Kwa urembo limefana, bali vitendo ni duni!
Kwanza nilipoliona, nilihisi burudani!
Bali uhai halina, lafisha kama tufani!
Nimepata nilidhani, kumbe nimepatikana!
Mmea huu mpana, na mingine hufanani!
Kwenye maji hapa mbona, unapataje madini?
Siutaki naukana, wavuvi tu vilioni!
Nimepata nilidhani, kumbe nimepatikana!
Wataishi vipi ngwena, na samaki mashakani?
Nasi ndo yetu hazina, kwa wenyeji na wageni
Madau, meli, safina, hazipiti abadani!
Nimepata nilidhani, kumbe nimepatikana!
Nani atapatikana, asiliye abaini?
Gugumaji kulichuna, viumbe kuviauni
Nema kichwa najikuna, nirudipo Msituni!
Nimepata nilidhani, kumbe nimepatikana!
DIWANI YA "MRATIBU", 2013.
Jisajili kwenye:
Chapisha Maoni (Atom)
Mambo ndiyo haya!!
JibuFuta