Jumatano, 14 Agosti 2013

NARUDI KWETU NARUDI

Nimechoka tangatanga, kila tengo nimefika!
Mithili mtu mjinga, vizuri asojiweka!
Yamenifinya majanga, utumwani kuteseka!
Kurudi kwetu nataka, duniya imenisonga!!!

Duniya imenisonga, kurudi kwetu nataka!
Kwa nini nilijitenga, na watu walosifika?
Kwangu huku kutochunga, kumenileta mashaka!
Kurudi kwetu nataka, nimekonda sina hali!!!

Nimekonda sina hali, kurudi kwetu nataka!
Hata usiku silali, naumu zimen'toweka!
Mavazi sina sijali, kufa nani anataka?
Kurudi kwetu nataka, nani atanikubali?

Nani atanikubali, kurudi kwetu nataka!
Chawa wamenikabili, damu yangu waitaka!
Kila mtu hanijali, viumbe vyanitoroka!
Kurudi kwetu nataka, ugenini kuna dhiki!


Kweli nimeisha hamu, narudi kwetu nyumbani!
Yamenichusha magumu, nilopata ugenini!
Nusura nife Kisumu, kwa maradhi kitandani!
Hata kama pawe duni, nyumbani kweli patamu!



Ola nilivoduwaa, sina wa kuniauni!
Hata nikiwa kazini, kamwe sikufurahia
Hata hivyo kazi gani, pato wanakukatia?
Sitaki kufanya deni, nianze kufatilia! 


Nyumbani ni nyumbani tu, hata kama ni chooni!
Siku nzima shinda njaa, pesa huna mfukoni!
Hata nikawe shujaa, magonjwa yapigwe nini?
Narudi kwetu nyumbani, ugeni sitakaa!


 DIWANI YA MRATIBU, 2013.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni