Wangoi wote malenga, watunzi wa kila fani
Naja nikipiga benga, ingawa nina huzuni
Leyo nyama naifunga, n'ole ata'yebaini
Hini ni kalamu gani, utakacho yaandika?
Ina nembo almasi, uchunguzapo makini
Ndaniye wino wa ngisi, haufutiki jamani
Yatumiwa na wakwasi, haifai masikini
Hini ni kalamu gani, utakacho yaandika?
Ukitaka rithi mke, uitowe mfukoni
Kisha nayo uandike, atakuja kiamboni
Lakini ubaya wake, kwa mke penzi huoni!
Hini ni kalamu gani, utakacho yaandika?
Ukihitaji mavazi, na mapambo muilini
Ujipake hina ngozi, waja wakakutamani
Bali sura h'igeuzi, kama u nyani u nyani
Hini ni kalamu gani, utakacho yaandika?
Utakacho itakupa, bali ina walakini!
Watu watakuogopa, 'kiwa nayo mkononi
Bali utatapatapa, kukosa utu insani
Hini ni kalamu gani, utakacho yaandika?
'Kiwa nayo husumbuki, licha zake nukusani
'Tapita kwenye bunduki, mitutu ya kila kani
Bali hayondoi chuki, kati yako na wendani
Hini ni kalamu gani, utakacho yaandika
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni