Ijumaa, 12 Aprili 2019

NITANENA

Kamwe sikomi kunena, maneno yenye maana
Nitanena kwa kudona, vimbwenga vinotubana
Nisiponena natuna, na moyo kujaa suna
Nitanena nikapona, kazi mbi ninaikana!

Nitayanena kwa kina, niuondowe uguna
Ninene mambo bayana, yanounga uungwana
Japo mtanitukana, nitukane kutukana
Nitanena nikapona, nyendo mbi nimezikana!

Sinyamazi nitanena, mdomo hujashikana
Msipotaka ninena, njoni kinywa mnishona
Ama mkatangamana, ili kushirikiana
Nitanena nikapona, ukabila naukana!

Maneno yana amana, walimu kwenda kwa wana
Hushauri kupatana, washari wakikinzana
Neno huleta fitina, na kwalo suluhu kuna
Nitanena nikapona, tuacheni kugombana!

Nitanena tena sana, ninene neno anana
Kwamba tuna kuungana, umoja na kupendana
Kwa marefu na mapana, tuisome Qur'ana
Nitanena nikapona, Biblia imenena!

Ugomvi, ushirikina, wizi, kuto'miniana
Ufisadi naukana, na ubakaji vimwana
Ujambazi hufishana, huleta ukata tena
Nitanena nikapona, nimepona nimena!

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni